JavaScript is required

Jinsi chekechea inavyofanya kazi (How kinder works) - Kiswahili (Swahili)

Chekechea, pia inajulikana kama 'shule ya chekechea' au 'elimu ya utotoni mapema', ni sehemu muhimu ya ukuaji na ujifunzaji wa mtoto wako. Kumuandikisha mtoto wako katika mpango wa chekechea kwa muda wa miaka miwili kunaweza kusaidia kukuza ujuzi wake ili kufanya vyema maishani na shuleni.

Saa za chekechea:

Programu za Chekechea wa Umri wa Miaka Mitatu ni za kati ya saa 5 na 15 kila wiki na programu za Chekechea wa Umri wa Miaka Minne ni za saa 15.

Matokeo yaliyothibitishwa:

Watoto wanaoenda kwenye programu ya chekechea huanza kukuza ujuzi kama vile jinsi ya kuhesabu na kutambua nambari na herufi, na jinsi ya kutatua matatizo. Mtoto wako atajenga kujiamini na kujitegemea huko chekechea na kujifunza stadi za kijamii na kihisia. Atashirikiana na kupata marafiki wapya.

Utafiti unaonyesha kuwa kwa umri wa miaka 16, wanafunzi ambao walikuwa wamehudhuria miaka miwili au 3 ya programu ya chekechea kabla ya kuanza shule walikuwa na alama za juu katika Kiingereza na hisabati kuliko wale ambao hawakuhudhuria.

Jinsi wazazi na waelimishaji wa chekechea hufanya kazi pamoja:

Chekechea hufanya kazi vizuri zaidi kama ushirikiano kati ya wazazi/walezi, familia na walimu. Kama mzazi/mlezi, wewe ndiye sehemu muhimu zaidi ya ukuaji wa mtoto wako. Unamfundisha mema na mabaya, lugha yako, utamaduni na maadili kama vile wema na heshima. Walimu watazungumza na wewe kuhusu kile kinachotokea chekechea na njia za kumsaidia mtoto wako kuendelea kujifunza nyumbani. Wanataka kujua kuhusu mambo anayopenda mtoto wako na jinsi anavyopenda kujifunza.

Unaweza kumwomba mwalimu wako wa chekechea kupanga mkalimani wakati wowote. Hii inaweza kuwa kwenye tovuti au kwa simu au video. Hakuna gharama inayohusika kwa familia kupata huduma hii.

Kinachotokea kwenye chekechea:

Walimu huhimiza watoto kujifunza kwa kucheza. Shughuli zinaweza kujumuisha kuchora, kuimba, kupanda, kuchimba na kukimbia nje, kucheza na vinyago na kusoma vitabu. Mchezo huwahimiza watoto kutumia mawazo yao na kufanya uvumbuzi, huku wakishirikiana na wengine kwa kushiriki na kupeana zamu kwa kufanya mambo. Watoto watajifunza kuhusu sauti, maneno na lugha, ikijumuisha jinsi ya kuzungumza na kuelewa Kiingereza.

Watoto wa chekechea ni sehemu ya jumuiya yetu ya tamaduni mbalimbali:

Programu za chekechea hukaribisha wazazi wa kutoka asili zote kuwa sehemu ya jumuiya zao. Ni mahali ambapo wazazi wanaweza kukutana na kushiriki hadithi na kujifunza kutoka kwa kila mmoja.

Walimu wanataka kujua kuhusu mtoto wako na utamaduni wako. Hii inawasaidia kuandaa programu ambazo ni za maana kwa mtoto wako, ikiwa ni pamoja na shughuli zinazozingatia siku za kitamaduni na matukio na kusherehekea utofauti katika Victoria.

Walimu hujumuisha kila mtu katika shughuli, kwa hivyo watoto ambao hawazungumzi Kiingereza wana fursa sawa za kucheza na kujifunza kama wengine. Baadhi ya programu za chekechea zina waelimishaji wa lugha mbili ambao huwasaidia watoto wanaozungumza Kiingereza kidogo au wasiojua kabisa. Watoto pia hufundishwa kupatana na kuwakubali wengine na kuheshimu tofauti za kiutamaduni.

Aina za programu za chekechea

Watoto wanaweza kuhudhuria programu ya Chekechea ya Umri wa Miaka Mitatu katika kituo cha matunzo cha siku ndefu (ambacho pia kinaitwa kituo cha kulelea watoto) au katika huduma ya chekechea ya pekee (ambayo pia huitwa huduma ya muda). Huduma hizi kwa kawaida hutoa pia programu ya Chekechea ya Umri wa Miaka Minne.

Kituo cha utunzaji wa siku ndefu kinaweza kutoa siku nzima ya elimu na utunzaji, pamoja na programu ya chekechea. Mpango wa chekechea unaoongozwa na mwalimu unaweza kuunganishwa na saa za ziada za elimu na utunzaji.

Katika huduma ya pekee, programu ya chekechea itafanya kazi tu kwa siku fulani na kwa nyakati maalum. Huduma ya pekee kwa kawaida hufanya kazi kwa wiki 40 kwa mwaka wakati wa muhula wa shule na kuchukua likizo kwa wakati uleule na shule. Siku hizi na saa zimewekwa na huduma ya chekechea.

Updated